WAZIRI ULEGA AIPONGEZA LST KWA KUBORESHA MAFUNZO.
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Abdallah Ulega ameipongeza Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (LST) kwa kuendelea na jitihada mbalimbali za kuboresha mafunzo ya uanasheria kwa vitendo ili kupata mawakili bora kwa maslahi ya taifa letu.
Akizungumza katika ziara yake alipotembelea LST leo Oktoba 15, 2026 Waziri Ulega aliwasisitiza viongozi na Watumishi kuendelea kufanya kazi kwa weledi, uwajibikaji na ubora ili kuhakikisha taifa linapata mawakili wenye viwango vya juu vya ubora vinavyoendana na wakati tulionao.
"Taasisi hii ndio chujio la mwisho katika kuwaandaa wanasheria kabla ya kwenda kufanya kazi za uanasheria, nawapongeza sana kwa kazi kubwa mnayoifanya na kwa kuzingatia umuhimu wa mafunzo yanayotolewa hapa, nawasihi kuhakikisha mafunzo hayo yanazingatia ubora unaotegemewa na Watanzania na walaji kwa ujumla wake", alisisitiza Waziri Ulega.
Aidha, katika ziara hiyo Waziri Ulega pia alipata fursa ya kuzungumza na wanafunzi wa LST na kuwasihi kutumia vyema wakati walionao pamoja na kuzingatia maendeleo ya teknolojia katika kujifunza na kuongeza maarifa kwa manufaa yao binafsi na maslahi ya taifa la Tanzania.
Kwa upande wake Mkuu wa Taasisi ya LST Prof. Sist Mramba alieleza kuwa Taasisi yake inajivunia mafanikio yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwake na kubainisha mikakati ya muda mfupi na mrefu iliyowekwa na Taasisi katika kuendelea kuboresha utoaji mafunzo ya uanasheria kwa vitendo.
Akifafanua kuhusu mafanikio, Prof. Mramba alisema kuwa tangu ilipoanzishwa hadi sasa LST imeweza kutoa wahitimu 11,217 sawa na asilimia 59 ya watahiniwa wote ambao wameongeza tija katika mnyororo wa utoaji haki nchini.
Pia alieleza kuwa LST imeimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa wanafunzi wanapokuwa kwenye mafunzo ya uwandani kwa kuanzisha matumizi ya mfumo wa kidigitali unaoitwa e-Field Management System.
"Mfumo wa e-Field umewezesha wakufunzi kuwafuatilia kwa usahihi wanafunzi sehemu wanapofanyia mafunzo ya uwandani (field) na pia umeboresha mawasiliano baina ya mkufunzi na mwanafunzi", alisema Prof. Mramba.
Pamoja na hayo Prof. Mramba alibainisha kuwa miongoni mwa mipango ya muda mrefu ya Taasisi ni pamoja na ujenzi wa Kituo cha Mafunzo Endelevu ya Kisheria (CLE) ambacho kitakuwa na sehemu maalum ya masuala ya usuluhishi (mediation and arbitration) itakayowezesha wanafunzi kujifunza kwa vitendo njia mbadala za umalizaji mashauri "Alternative Dispute Resolution".
Waziri Ulega ametembelea LST kwa lengo la kufahamu majukumu ya taasisi hiyo ambapo aliambatana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Mhe. Balozi Baraka Luvanda pamoja na baadhi ya wakurugenzi wa wizara hiyo.
