Historia
Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (The Law School of Tanzania) ilianzishwa kwa Sheria ya Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo, (The Law School of Tanzania Act) Sura ya 425 ya mwaka 2007. Lengo la kuanzishwa kwa Taasisi ni kuandaa, kuendesha na kutoa mafunzo ya uanasheria kwa vitendo kwa wahitimu wa shahada ya kwanza ya sheria ambao wangependa kufanya kazi kama wanasheria katika Utumishi wa Umma au kufanya kazi ya uwakili wa kujitegemea. Kuanzishwa kwa Taasisi kulifuta mfumo wa ‘internship’ uliokuwa ukitumika nchini tangu mwaka 1974 na ambao ulionekana kuwa na mapungufu katika kuwaandaa wanasheria kufanya kazi zao za kisheria. Mfumo huu ulikoma tarehe 2 Mei, 2007. Chini ya utaratibu huo wahitimu wa Shahada ya Sheria walitakiwa kufanya mafunzo kwa vitendo katika moja ya taasisi zifuatazo: - Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mahakama ya Tanzania na Shirika la Sheria Tanzania ili kuwa na sifa za kufanya kazi ya uwakili. Hivyo, mafunzo haya ni fursa kwa wahitimu wa shahada ya kwanza ya sheria kupata stadi na ujuzi wa kutekeleza majukumu mbalimbali ya uanasheria.
Msingi wa kuanzishwa kwa Taasisi hii ni mapendekezo ya taarifa ya Tume ya Jaji Mark Bomani, Tanzania Financial and Legal Management Upgrading Project, Legal Sector Report, 1996 maarufu kama Ripoti ya Bomani. Kwa mujibu wa taarifa ya Tume ya Bomani, kuanzia mwaka 1992 na kurudi nyuma, wahitimu wote wa shahada ya kwanza ya sheria walitakiwa kwa mujibu wa sheria kufanya kazi katika utumishi wa umma kwa kipindi kisichopungua miaka mitano mara baada ya kuhitimu masomo yao. Kimsingi hiki kilikuwa ni kipindi cha mafunzo ya sheria kwa vitendo chini ya usimamizi wa wanasheria wazoefu waliokuwa kwenye utumishi wa umma.
Baada ya mwaka 1992, Serikali ilifuta utaratibu uliokuwepo ikiwa ni pamoja na kujivua wajibu wa kuwapatia wahitimu wa shahada ya sheria sehemu za kufanyia mazoezi katika Utumishi wa Umma. Matokeo ya uamuzi huo wa Serikali yalikuwa ya aina kuu mbili: (i) Tanzania ilijikuta ikiwa haina mfumo rasmi wa kutoa mafunzo kwa vitendo kwa wahitimu wa shahada ya kwanza ya sheria, kama zilivyo nchi nyingi za Jumuiya ya Madola; na (ii) wahitimu wengi wa shahada ya sheria walikosa sifa muhimu “internship” ili kukidhi masharti ya kusajiliwa kuwa mawakili. Aidha, utaratibu wa “internship” kwa kipindi cha miezi sita uliokuwa unaratibiwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ulimudu kutoa nafasi kwa wahitimu wachache tu waliobahatika. Hivyo, Tume ilipendekeza ifuatavyo:- ‘Tanzania needs a formal system of vocational training for graduates’ ikiwa na maana kwamba Tanzania inahitaji mfumo rasmi wa mafunzo ya vitendo kwa wahitimu wa sheria. Taarifa ya Jaji Bomani (p.17) inabainisha athari zinazotokana na mfumo wa “Internship” kuwa ni pamoja na:
- Tanzania kuwa na mfumo tofauti wa kuandaa na kusajili wanasheria kuwa mawakili ikilinganishwa na nchi nyingine za Jumuiya ya Madola, kama vile Kenya, Uganda na Ghana;
- Kipindi cha miezi sita cha “internship” kilikuwa hakina ufanisi na hakitoshelezi kwa wahitimu wa shahada ya kwanza ya sheria kuendesha shughuli za uwakili;
- Mfumo wa “internship” uliwapendelea wahitimu ambao walibahatika kuendelea na ajira katika utumishi wa umma na hivyo kuwa na fursa zaidi ya kupata uzoefu na mafunzo kazini. Kwa wengine waliokosa nafasi katika utumishi wa umma hawakuwa na fursa nyingine na hivyo kukosa sifa za kusajiliwa kama mawakili;
- Ni dhahiri kwa mfumo wa hapo awali Tanzania ingeendelea kukabiliwa na tatizo la uhaba wa wanasheria wenye ujuzi katika maeneo mbalimbali ya kiuchumi na kijamii (haki za binadamu, uandishi wa sheria, majadiliano ya mikataba ya kibiashara na mikataba ya kimataifa) na hivyo kuwa ni kinyume na sera za Serikali kuhusu maendeleo;
- Kutokana na utaratibu wa “internship” kuwa na malengo ya muda mfupi, ni dhahiri kwamba Tanzania ingeendelea kutokuwa na mfumo rasmi wa utoaji wa mafunzo ya uanasheria kwa vitendo;
- Kukosekana kwa taasisi mahsusi kwa ajili ya mafunzo endelevu (CLE) kwa wanasheria.
Baada ya kuona umuhimu wa kuondoa utaratibu wa “internship”, Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo ilianzishwa kwa lengo la kuandaa, kuendesha na kutoa mafunzo ya uanasheria kwa vitendo kwa wahitimu wa shahada ya kwanza ya sheria ambao wangependa kufanya kazi kama wanasheria katika utumishi wa umma au kufanya kazi ya uwakili wa kujitegemea. Kuanzishwa kwa Taasisi hii kulifuta mfumo wa “internship” uliokuwa ukitumika nchini tangu mwaka 1974 na kukoma tarehe 2 Mei, 2007. Hivyo, mafunzo haya ni fursa kwa wahitimu wa shahada ya kwanza ya sheria kupata stadi na ujuzi wa kutekeleza majukumu mbalimbali ya kisheria.
Mfumo wa kutoa mafunzo ya uanasheria kwa vitendo umekuwa ukitumiwa na nchi za Jumuiya ya Madola kama vile Ghana, Kenya, Uganda na Afrika ya Kusini. Uzoefu kutoka nchi hizo unaonesha kuwa chini ya mfumo huu nchi hizo zimefanikiwa katika kujenga uwezo na kuwapa stadi za kazi wahitimu wa sheria kutoka vyuo vikuu na hivyo kuweza kukidhi mahitaji ya soko la ajira mara baada ya kuhitimu. Pia, idadi ya wanasheria wenye ujuzi katika nchi hizi imekuwa ikiongezeka kwa haraka kutokana na uwezo wa kupokea wanafunzi wengi kwa wakati mmoja.
Kuongezeka kwa idadi ya vyuo vinavyotoa Shahada ya Kwanza ya Sheria nchini Tanzania kulipelekea kuwepo kwa mahitaji makubwa ya mafunzo ya uanasheria kwa vitendo ambapo uwezo wa taasisi zilizokuwa zinatoa mafunzo hayo uliendelea kubaki vilevile. Aidha, utaratibu wa “internship” ulikuwa hautoi fursa za kutosha kwa wanafunzi kukutana na wasimamizi wa sehemu za kazi kwa ajili ya kupokea maelekezo na kupata ufafanuzi katika baadhi ya masuala. Hivyo, Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania imeweza kwa kiasi kikubwa kuziba pengo la nafasi na fursa ya kujifunza lililokuwepo.
Baada ya kuanzishwa kwa Taasisi hii, mafunzo yalianza rasmi tarehe 27 Machi, 2008 ambayo yalizinduliwa na Mhe. Mathias M. Chikawe (MB), Waziri wa Katiba na Sheria wa wakati huo. Mafunzo yalikuwa yakifanyika katika Majengo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na hii ilikuwa ni kwa sababu Taasisi ilikuwa haina majengo yake. Kutumika kwa majengo ya chuo hicho katika kufundishia ilikuwa ni kwa mujibu wa Mkataba Maalum uliosainiwa na Taasisi na Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam. Kupitia jitihada hizo, jumla ya wanafunzi 274 walisajiliwa na kupata mafunzo katika Kundi la Kwanza.
Uongozi wa Taasisi ulipewa Ofisi za muda katika Ofisi za Programu ya Maboresho ya Sekta ya Sheria nchini (Legal Sector Reform Programme-LSRP) zilizokuwa Ghorofa ya Pili, Jengo la Sukari, Sokoine Drive/Mtaa wa Ohio, Dar Es Salaam. Taasisi ilihamia katika Ofisi zake za muda katika Jengo la Ubungo Plaza, mkabala na Barabara ya Morogoro, Dar Es Salaam mwezi Februari, 2009 baada ya LSRP kuipatia samani, vifaa na raslimali fedha za kuanzisha ofisi. Wizara ya Katiba na Sheria kupitia LSRP iliipatia Taasisi majengo na miundombinu kupitia LSRP kati ya Novemba 2010 na Juni 2013 kwenye Kampasi yake yenye eneo la ekari 23 katika Kiwanja Na. 2005/02/01, Kitalu ‘C’, Sinza, Ubungo, Dar Es Salaam. Katika awamu ya kwanza, majengo yaliyojengwa ni pamoja na Jengo la Kufundishia, Jengo la Utawala, Maktaba, Ukumbi wa Mikutano na Shughuli Mbalimbali, Mahakama ya Kujifunzia, Jengo la Mgahawa wa Watumishi na Jengo la Makazi ya Watumishi. Vilevile, kuna barabara ya ndani, viwanja vya michezo na uzio kuzunguka eneo lote la Taasisi. Uwepo wa majengo haya umewezesha kuongeza udahili wa wanafunzi kutoka wastani wa wanafunzi 600 kwa mwaka hadi 1,800.