WAZIRI DR. HOMERA ATEMBELEA LST
WAZIRI DR. HOMERA ATEMBELEA LST
24 Dec, 2025
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Homera amekabidhi magari matatu kwa Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (LST) ikiwa ni hatua ya kuendelea kuboresha miundombinu ya Taasisi hiyo.
Waziri Homera amefanya makabidhiano hayo tarehe 12 Desemba, 2025 alipotembelea LST kwa ziara ya kikazi akiwa ameambatana na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Zainab Katimba pamoja na Naibu Katibu Mkuu Dkt. Franklin Rwezimula.
Katika ziara hiyo Waziri Homera alipata fursa ya kuzungumza na Menejimenti ya Taasisi pamoja na Watumishi ambapo aliwasisitiza kuendelea kuchapa kazi kwa bidii na weledi ili kuzalisha wanasheria wengi mahiri wenye uadilifu kwa maslahi ya Taifa letu.
Kwa upande wake Mkuu wa Taasisi ya LST, Prof. Sist Mramba alitoa shukrani za dhati kwa Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuendelea kuiwezesha LST katika masuala mbalimbali ikiwemo kuboresha miundombinu ya utendaji kazi na maslahi ya watumishi.
Aidha alibainisha kuwa LST itaendelea kutoa mafunzo ya sheria kwa vitendo kwa kuzingatia ubora, weledi na maadili.
