Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (LST)

lst Logo
LST YASHIRIKI KUTOA ELIMU KWENYE WIKI YA SHERIA
07 Feb, 2024
LST YASHIRIKI KUTOA ELIMU KWENYE WIKI YA SHERIA

Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (LST) imeendelea kutoa elimu na ushauri wa masuala ya kisheria kwa wadau na wananchi mbalimbali wanaotembelea maonesho ya Wiki ya Sheria yanayofanyika kitaifa katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma kuanzia tarehe 24-27 Januari, 2024.

Maonesho hayo ambayo yamezinduliwa rasmi na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson yametanguliwa na matembezi maalum ambayo yalishirikisha viongozi mbalimbali wa Mahakama, watumishi wa umma na wananchi kutoka jiji la Dodoma.

Kwa kuzingatia kaulimbiu ya mwaka huu inayosema “Umuhimu wa Dhana ya Haki kwa Ustawi wa Tanzania: Nafasi ya Mahakama na Wadau katika Kuboresha Mfumo Jumuisho wa Haki Jinai”, lengo la maonesho hayo ni kuziweka pamoja taasisi zote za haki jinai ili ziweze kubadilishana uzoefu na kuona njia bora ya utendaji kazi kwa pamoja katika utoaji haki kwa wananchi. Aidha, yanawezesha wananchi kutembelea taasisi zote za haki jinai na kuweza kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya kisheria kupitia taasisi hizo.

 

Mhadhiri wa LST, Dkt. Kevin Mandopi ambaye anashiriki kutoa elimu katika banda la Taasisi hiyo amesema kuwa LST inashiriki kikamilifu kwa kutumia fursa hiyo kutoa ufafanuzi kuhusu majukumu yake, kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala mbalimbali ya sheria hususan yanayohusu haki jinai pamoja na kutoa ushauri wa kisheria kwa wananchi wenye uhitaji.

 

Kwa upande wao wananchi wanaotembelea maonesho hayo wameipongeza Mahakama kwa kuandaa maonesho na taasisi zinazoshiriki kutoa elimu ya sheria kwa Watanzania, pia wamefurahia huduma na ushauri wanaopata kutoka kwa washiriki hao.

 

Maonesho hayo yanatarajiwa kuhitimishwa rasmi jijini Dodoma na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan mnamo tarehe 1 Februari, 2024 ambayo ni siku ya kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Sheria.

Online Help
Kuanzisha Enzi Mpya katika Udhibiti wa Sekta ya Michezo ya Kubahatisha nchini Tanzania
https://saris.lst.ac.tz/Registrations

" >